28 Januari 2021

MKUU WA WILAYA YA ILALA AKAGUA MASOKO KATA YA LIWITI

 Na,Judith Damas,Mariam Hassan na Exsebia.


Mkuu wa Wilaya Ya Ilala Mh.Ng’wilabuzu Ludigija ametoa maagizo kwa wafanyabiashara wote wa masoko ya Bombom, Minazi Mirefu na Kigilagila  ifikiapo tarehe 8 Februari 2021 wawe wameahamia kwenye masoko hayo mapya na pia atagawa  vizimba kwa  kila mmoja wao. 

Amesema hayo katika ziara yake ya kukagua ukamilikaji wa ujenzi wa masoko hayo akiambatana na Katibu tawala wa Wilaya ya Ilala na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala na Mkuu wa Masoko Manispaa ya Ilala leo tarehe 27 Januari 2021.

 “Ninawaomba muwe wavumilivu zoezi litafanyika kwa siku tano hadi kufikia tarehe 8 February 2021 nitawagawia vizimba kulingana na Orodha ya wafanyabiashara kupitia jina kwa jina na kila mmoja awe na kitambulisho cha Mpiga kura au Taifa.”

 

                Mkuu wa Wilaya ya Ilala akiongea na wafanya biashara wa soko la BOMBOM


Pia, Mkuu wa Wilaya ameipongeza Serikali kwa miundombinu mizuri ambayo itawasaidia  wafanyabiashara kusafirisha mizigo yao kiurahisi.

 “Naipongeza Serikali ya awamu ya tano kwa miundombinu mizuri hivyo nawasihi mlinde miundombinu na kutunza mazingira ili kuepuka magonjwa ya milipuko

Hata hivyo, Mh. Ludigija amewaasa wafanyabiashara waache tabia ya kupangisha fremu  na atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.

Mwenyekiti wa Soko la Bombom Bw. Muhidini Waziri ameishukuru Serikali  pamoja na Manispaa ya Ilala kwa kuwajengea soko la kisasa kwani awali soko hilo lilikuwa linajaa maji kipindi cha mvua hivyo biashara inakuwa ngumu na kina mama walikuwa wanapata tabu kuingia sokoni.

Vilevile Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Ndug. Jumanne Shauri amesema kujengwa kwa masoko hayo inapunguza adha kwa wananchi kusafiri sehemu za mbali kwenda kuchukua bidhaa.

Aidha, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala alisema kutokana na kodi inayopatikana katika masoko hayo inasaidia uwepo wa huduma nyingine za kijamii.

“Sisi kama Manispaa ya Ilala tuna takribani masoko 36 hivyo kutokana na kodi inayotolewa inasaidia kujenga madarasa na vituo vya afya”

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni