17 Februari 2021

Madiwani Ilala wapitisha taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2020

Na: Judith Damas

 Halmashauri ya Manispaa ya Ilala  imetekeleza miradi ya maendeleo katika kata zake ili kuhakikisha huduma zote za kijamii zinawafikia wananchi wake kwa uharaka zaidi na pia kuhakikisha suala la ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala linatekelezwa kikamilifu.

Hayo yamebainishwa na wenyekiti wa kamati za kudumu za Halmashauri wakati wakiwasilisha taarifa za Miradi ya maendeleo iliyotekelezwa na Manispaa ya Ilala kwa kipindi cha kuanzia oktoba 2020 hadi Disemba  2020 katika kikao cha Baraza la Madiwani cha robo ya pili cha kupitia taarifa za utendaji kazi kilichofanyika leo tarehe 17 februari 2021 katika ukumbi wa Mikutano wa Arnatouglou-Mnazi Mmoja Jijini Dar es salaam.
Aidha, akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi ya kamati ya fedha na utawala kwa niaba ya mwenyekiti wa kamati hiyo Mh.Saady Khimji, amesema kwa kipindi cha robo ya pili, Manispaa ya Ilala imeweza kutekeleza miradi mbalimbali ya kimaendeleo kama  vile ujenzi wa soko la kisutu, ujenzi wa  vyumba vya madarasa, ujenzi wa zahati ya Bangulo na pia ujenzi wa barabara mbalimbali za mitaa kupitia mradi wa   DMDP Manispaa ya Ilala ili kuhakikisha huduma zote za kijamii zinawafikia wananchi kiurahisi zaidi.

Hata hivyo, Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imefanikiwa kupunguza maambukizi ya ugonjwa wa malaria kwa wamama wajawazito na pia kununua dawa muhimu zitakazoweza kuwakinga mama na mtoto, hayo yamesemwa na  mwenyekiti wa kamati ya uchumi na huduma za jamii Mh.Stephen Mushi wakati akiwasilisha taarifa ya utendajin kazi ya kamati hiyo.

Pamoja na hayo, kamati ya uchumi na huduma za jamii imeanzisha vikundi 120 kwa ajili ya kuwapa fursa watu wasio na ajira hususani vijana, wanawake na watu wenye ulemavu katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilala kwa kuwapatia mikopo isiyokuwa na riba.

Vilevile, Halamshauri ya Manispaa ya Ilala imeendelea kuhakikisha maeneo yake yote yanakuwa masafi kwa kuanza kutoa elimu ya umuhimu wa usafi wa mazingia ambayo imekuwa ikitolewa kwa wananchi wa Maniaspaa ya Ilala ili kuhakikisha wanatunza mazingira na kuyaweka katika hali ya usafi kwa ajili ya kulinda afya zetu, hayo ameyasema mwenyekiti wa kamati ya mipango miji na mazingira Mh. Sultan Salim.

Kikao cha Baraza la Madiwani kilipitia taarifa hizo na kuzipitisha

28 Januari 2021

MKUU WA WILAYA YA ILALA AKAGUA MASOKO KATA YA LIWITI

 Na,Judith Damas,Mariam Hassan na Exsebia.


Mkuu wa Wilaya Ya Ilala Mh.Ng’wilabuzu Ludigija ametoa maagizo kwa wafanyabiashara wote wa masoko ya Bombom, Minazi Mirefu na Kigilagila  ifikiapo tarehe 8 Februari 2021 wawe wameahamia kwenye masoko hayo mapya na pia atagawa  vizimba kwa  kila mmoja wao. 

Amesema hayo katika ziara yake ya kukagua ukamilikaji wa ujenzi wa masoko hayo akiambatana na Katibu tawala wa Wilaya ya Ilala na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala na Mkuu wa Masoko Manispaa ya Ilala leo tarehe 27 Januari 2021.

 “Ninawaomba muwe wavumilivu zoezi litafanyika kwa siku tano hadi kufikia tarehe 8 February 2021 nitawagawia vizimba kulingana na Orodha ya wafanyabiashara kupitia jina kwa jina na kila mmoja awe na kitambulisho cha Mpiga kura au Taifa.”

 

                Mkuu wa Wilaya ya Ilala akiongea na wafanya biashara wa soko la BOMBOM


Pia, Mkuu wa Wilaya ameipongeza Serikali kwa miundombinu mizuri ambayo itawasaidia  wafanyabiashara kusafirisha mizigo yao kiurahisi.

 “Naipongeza Serikali ya awamu ya tano kwa miundombinu mizuri hivyo nawasihi mlinde miundombinu na kutunza mazingira ili kuepuka magonjwa ya milipuko

Hata hivyo, Mh. Ludigija amewaasa wafanyabiashara waache tabia ya kupangisha fremu  na atakayebainika atachukuliwa hatua za kisheria.

Mwenyekiti wa Soko la Bombom Bw. Muhidini Waziri ameishukuru Serikali  pamoja na Manispaa ya Ilala kwa kuwajengea soko la kisasa kwani awali soko hilo lilikuwa linajaa maji kipindi cha mvua hivyo biashara inakuwa ngumu na kina mama walikuwa wanapata tabu kuingia sokoni.

Vilevile Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Ndug. Jumanne Shauri amesema kujengwa kwa masoko hayo inapunguza adha kwa wananchi kusafiri sehemu za mbali kwenda kuchukua bidhaa.

Aidha, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala alisema kutokana na kodi inayopatikana katika masoko hayo inasaidia uwepo wa huduma nyingine za kijamii.

“Sisi kama Manispaa ya Ilala tuna takribani masoko 36 hivyo kutokana na kodi inayotolewa inasaidia kujenga madarasa na vituo vya afya”

 

 

 

25 Januari 2021

Mkuu wa Wilaya ya Ilala azitaka mamlaka kusuluhisha mgogoro Bonde la Mto Msimbazi

 Na, Judith Damas

 Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mh. Ng’wilabuzu  Ludigija ameziagiza taasisi za Serikali zikiwemo NEMC, TARURA, TANROAD, Bonde la mto wami  na idara ya Mazingira Manispaa ya Ilala kukutana na kuweza kujadiliana kuhusu zoezi la kutengeneza kingo katika bonde la Msimbazi.

Mkuu wa Wilaya Mh. Ludigija ameyasema hayo leo  tarehe 25  Januari 2021 alipokutana na wananchi wa Kata ya Kipawa mtaa wa Stakishari katika ziara yake ya kutembelea bonde hilo la Msimbazi ambalo limeleta changamoto kwa wananchi wa mtaa huo wakilalamika kuhusu zoezi hilo la kutengteneza bonde hilo  linavyofanyika .

Aidha wananchi wa eneo hilo  wakitoa malalamiko yao kwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mh.Ng’wilabuzu Ludigija juu ya zoezi hilo linavyowaletea madhara makubwa ikiwemo mafuriko, kuharibika kwa miundombinu kama  barabara zao na kusababisha uharibifu wa miundombinu ya umeme kwani magari yanayopita katika eneo hilo ni makubwa na yanabeba mzigo mkubwa.

Akipokea hoja hizo za wananchi Mkuu wa Wilaya ya Ilala amewaomba wananchi hao wawe wavumilivu hadi taasisi hizo zitakapo kutana na kujadiliana kuhusu zoezi hilo.

“Naagiza taasisi  zote za Serikali ikiwemo TARURA,NEMC,TANROAD,Bonde la mto wami na idara ya mazingira Manispaa ya Ilala zikutane na zijadiliane kama zoezi hili linalofanyika lina tija katika kuzuia mmomonyoko na mafuriko,  na ifikapo Ijuumaa January 29/2021 nipate mrejesho kama zoezi hilo liendelee au lisitishwe ili kuzuia athari zitakazotokea”.amesema  hayo mkuu wa wilaya ya Ilala Mh. LudigijaMto Msimbazi

Aidha Mkuu wa wilaya ya Ilala Mh.Ng’wilabuzu Ludigija ameongezea kuwa ikibainika kama zoezi hilo lina tija kwa wananchi wa stakishari waliozungukwa na bonde la mto msimbazi taasisi hizo zikae na wananchi hao na kuwapa maelekezo juu ya umuhimu wa zoezi hilo ili waweze kuridhika na kutoa maoni yao.

Kwa upande wa Afisa mazingira Ndug.Shabani Manzi  amesema kuwa kitu kikubwa wanachokifanya ni kuzuia mmomonyoko wa ardhi na mafuriko kipindi cha mvua, hivyo anaamini zoezi hilo lina tija kwa wanaanchi wa maeneo hayo.Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mh. Ng'wilabuzu Ludigija akiwa na wataalamu kutoka Manispaa ya Ilala wakikagua Mto Msimbazi


“Tulikutana na wawakilishi wa wananchi wakatuomba tuweke kingo katika bonde la mto msimbazi ili kuepuka athari zinazojitokeza kipindi cha mvua, naamini wananchi wote wanapenda zoezi hilo lifanyike ila hawapendezwi na namna ya zoezi hilo linavyofanyika hivyo tunawaahidi tutalifanya zoezi hilo ipasavyo”. Amesema hayo Ndug.Shabani Manzi.

Akiwatoa hofu wananchi wakazi wa stakishari Ndug. Zakayo Mgaya mmojawapo wa kampuni ya ORAL INVESTIMENT, amesema kuwa baada ya zoezi hilo kukamilika watahakikisha wanatengeneza barabara hizo na kuacha mazingira salama.

7 Januari 2021

Mkurugenzi Manispaa ya Ilala awaagiza Walimu Wakuu sekondari kukamilisha ujenzi wa madarasa

 Na Judith Damas na Mariam Hassan

Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa ya Ilala Bw. Mussa Ally amewahimiza walimu wakuu kutimiza wajibu na kuwa na ushirikiano baina yao wenyewe na viongozi wao wa kata ili kuboresha ufaulu,  Ameyasema hayo leo tarehe 7/1/2021 katika kikao kazi cha kufanya maandalizi rasmi ya ufunguzi wa Shule kilichofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Tambaza.
Afisa Elimu Sekondari Bw. Mussa Ally
 Baadhi ya walimu wakuu wa shule za sekondari za Manispaa ya Ilala waliofika katika kikao kazi hicho wakisikiliza kwa makini


Vilevile Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Ndug. Jumanne Shauri ameongezea kuwa kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa pamoja na madawati hivyo Halmashauri yatoa zaidi ya billioni nne kwa ujenzi wa madarasa na ukarabati wa madawati ili kuhakikisha ifikapo february 28 wanafunzi wote wa sekondari Wilaya ya Ilala wanaingia darasani bila changamoto yoyote.
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Ndg. Jumanne Shauri akihotubia


Pia, amewasisitiza Walimu wakuu wote, Maafisa Elimu Kata, Madiwani na Watendaji wa Kata kufanya kazi kwa kushirikiana kwa amani na uelewano baina yao.

Mgeni rasmi Mstahiki Meya Manispaa ya Ilala Mh. Omari Kumbilamoto amewaahidi Wakuu wa Shule pamoja na Maafisa Elimu Kata amewaahidi kuwapa ushirikiano kwa lolote litakalotokea atahakikisha atapambana nalo ili idara ya Elimu Sekondari kufanya vizuri.
Meya wa Manispaa ya Ilala Mh. Omari Kumbilamoto


Mwalimu Mkuu Shule ya Sekondari Tambaza Bw. Husein Zuberi Mavumba ametoa shukrani kwa Mkurugenzi na Mstahiki Meya kwa kuwaahidi watafanya kazi kwa bidii na kasi kubwa sana.

30 Desemba 2020

Mhe. Nderiananga azihimiza Halmashauri kutoa mikopo kwa wakati

 Na: Hashim Jumbe

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu wenye ulemavu) Mhe. Ummy H. Nderiananga amezihimiza Halmashauri zote nchini kutoa kwa wakati mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu ili kuwarahisishia kuendesha biashara zao.

Hayo ameyasema leo katika ukumbi wa mikutano wa Arnatouglou uliopo Manispaa ya Ilala katika kikao kazi na Maafisa Ustawi, Maafisa Maendeleo na Maafisa Vijana wa Halmashauri zote za Jiji la Dar es Salaam

"Dhamira na nia ya Serikali ni njema sana kwa kundi la watu wenye ulemavu, vijana na wanawake na mwanzoni mnakumbuka ilikuwa wanawake 5% na vijana 5%, Serikali ikaja ikafanya maboresho ikasema sasa tunaweka wanawake 4%, vijana 4% na walemavu 2%, hapa ninachoona kwa pamoja tukishirikiana kama ambavyo tulivyoanzia 0% mpaka asilimia fulani tuendelee kuongeza kasi"

Aidha, Mhe. Nderiananga aliwahimiza watumishi hao kurahisisha upatikanaji wa mikopo kwa makundi hayo huku akisisitiza lengo la Serikali ni kuwaletea maendeleo wananchi wake "Maafisa Maendeleo, Maafisa Ustawi na Maafisa Vijana tusaidiane ili tuweze kurahisisha upatikanaji wa mikopo ili vikundi vingi na watu wengi wenye uhitaji kunufaika na mikopo hii"

13 Desemba 2020

UONGOZI NA DIRA YA MAENDELEO

 Na Mwandishi wetu

Uongozi ni mamlaka au karama anayopewa mtu kuwaonyesha watu njia kwa vitendo. Kipimo cha uongozi ni namna ambavyo kiongozi anaweza kuleta ushawishi kwa watu na kufikia maendeleo yaliyotarajiwa.

Katika matoleo ya jarida hili tutakuwa na mfululizo wa makala kuhusu uongozi kama itakavyokuwa ikizungumziwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Bw. Jumanne Shauri. Hii ni sehemu ya kwanza ya makala hiyo; 

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Bwana Jumanne Shauri anaanza kwa kuongelea namna ambavyo kiongozi bora anatakiwa kuwa ili kufanikisha malengo yake anayoyapanga katika kuhudumia  watu anaowaongoza.

Akihojiwa na mwandishi wa jarida hili Mkurugenzi amesema kiongozi lazima awe na dira itakayo muwezesha kupanga mpango mkakati ili kukamilisha dira hizo kwani viongozi waliofanikiwa  hutengeneza dira na kufanikiwa katika uongozi wao kupitia dira walizoziweka.

Dira ni nini?

Dira ni kifaa cha kutambua mwelekeo hivyo dira inapaswa kuonesha muelekeo wa kiongozi wapi alipotoka na ndoto anazotaka kuzifikia. Dira ndio nguzo kuu ya kiongozi itakayo mwezesha kufanikisha malengo yake kupitia mipango ya kimkakati atakayo iweka kwa kulinganisha dira yake na ndoto zake.

Na sio  tu kwa kiongozi bali mtu yoyote ili afanikiwe malengo yake lazima awe na dira na ndoto ili apate muelekeo wa nini anakitaka kukifikia na pia kutengeneza mikakati ya kufikia jambo lake. Katika kuliongelea hilo Bwana Shauri alisema “hata wanafunzi wakitaka kufaulu masomo yake lazima aweke dira kwamba anataka kufikia ufaulu gani mathalani ufaulu wa daraja la kwanza kisha aweke mikakati ni namna gani anaweza kufikia mafanikio hayo”.

Pia Mkurugenzi anasema ” mtu huwezi kukurupuka tu na kusema leo unataka kukimbia mbio za riadha kama hauna maandalizi hivyo ni lazima ujiandae kwa muda hata miezi sita au  ndani ya mwaka mmoja ndipo uweze kushiriki riadha na kufanikiwa kushinda”

 

DIRA ZA VIONGOZI TANZANIA

Tangu awamu ya kwanza ya uongozi wa nchi Tanzania, viongozi wake wote walikua na dira waliozitumia katika kuhudumu muda wote wa uongozi wao na kufanikisha mengi kwa kufuata dira hizo.

Tangu nchi ipate uhuru mpaka sasa Tanzania ina awamu tano za uongozi na awamu zote viongozi wake walihudumu kwa mafanikio makubwa kwa kutumia dira za maendeleo na mipango ya kimkakati ya kufikia dira hizo

Awamu ya kwanza ya uongozi Tanzania chini ya Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ulikua na dira ya kupiga vita umasikini, maradhi na ujinga ili kuhakikisha kila mtanzania anakua na maisha bora.

Dira hiyo ilifanikiwa na kuwafanya wananchi kuondokana na ujinga kwa kufanya elimu kuwa bure ili watanzania wote waweze kusoma hata kama wana hali ya umasikini. Watoto pia walipata nafasi ya kufundishwa na walimu wa UPE  na kupata elimu ya msingi iliyowasaidia kujua kusoma na kuandika.mwalimu Julius Nyerere aliamzisha elimu ya kujitegemea kuanzia shule za msingi mpaka sekondari na vyuoni huku lengo la elimu hiyo likiwa ni kuondoa ujinga pamoja na kuwafanya watanzania wasiwe wageni wa mazingira yao na kuyatumia vyema ili kuweza kujiingizia kipato kwa shughuri mbalimbali za kiuchumi kama kilimo, uvuvi pamoja na useremala.

 

Katika suala la kuondoa umasikini Mwalimu Nyerere alianzisha taasisi ya chakula na lishe. Mapema kabisa wakati Dunia ikiwa bado haijui mchango wa lishe bora kwa watoto na hapa Afrika Tanzania ilikuwa nchi ya kwanza kabisa kuanzisha kituo maalumu cha kutafiti na kuishauri serikali juu ya lishe ya watoto na watu wake kwa ujumla (Tanzania Food and Nutrition Centre). Mpaka leo Tanzania inaheshimika duniani kote kwa kuwa na wataalamu wabobezi katika lishe. Mataifa mengi duniani kote huja hapa nyumbani kujifunza namna kituo chetu cha chakula na lishe kinavyochagiza mipango makini ya afya ya ulaji serikalini na kwa wananchi

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Mseru amewahi kusema kuwa mwalimu Julius Nyerere ndio muasisi wa bima ya afya ya jamii mwaka 1962.Profesa Mseru ameeleza hayo Oktoba 11, 2019 wakati akizungumza katika kongamano la siku mbili la  kumbukizi ya Mwalimu Nyerere lililoandaliwa na taasisi ya uongozi kwa ushirikiano na  UDSM. Amesema japo Serikali wakati huo hakikuwa kubwa kama sasa, lakini Nyerere alijua mahitaji ya wananchi  na changamoto wanazozipata katika  matibabu yao kwa kutokuwa na utaratibu huo. .

Lakini pia katika kupigana vita na adui umasikini mwalimu julius kambarage Nyerere  alianzisha falsafa ya ujamaa na kujitegemea lengo kuu la falsafa hii lilikuwa ni kulifanya taifa la Tanzania kuwa na uchumi wa kujitegemea na kutokuwa ombaomba kwa mabeberu. Kufuatia dhima hiyo mwalimu nyerere alikuja na mipango mkakati mbalimbali ya kuhakikisha sera ya ujamaa na kujitegemea inaikia malengo kwa kumfaidisha kila mtanzania ambapo alianzisha mipango mbalimbali ikiwemo mashamba ya vijiji, pamoja na kuanziaha viwanda ili kuwezesha upatikanaji wa ajira miongoni mwa watanzania ili kuweza kupata kipato cha kujikimu kimaisha.

 

kwa upande wa Rais Mstaafu wa awamu ya pili Mhe. Ally Hassan Mwinyi alikuja na Dira ya kuikomboa nchi katika hali mbaya ya kiuchumi ya nchi yetu kutokana na athari ya vita ya Kagera wakati huo hiyo kuja na kauli mbiu ya RUKSA. Dira hiyo iliangazia kupigania wanyonge na watu wa hali ya chini kwani alitoa ruksa kwa shughuli zote halali zilizokatazwa kufanywa kufanyika bila kuvunja sheria za nchi. Dira hiyo ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa.

Rais wa awamu ya tatu Hayati Benjamin Mkapa yeye aliongoza Tanzania chini ya Sera ya ubinafisishaji akilenga Taifa la Tanzania liweze kuingia katika uchumi wa kati katika maendeleo yake. Akiwa madarakani Rais Mkapa alibinafsisha baadhi ya mashirika yanayomilikiwa na Serikali na akatumia sera ya soko huru. Dira yake ilipata msaada wa Benki ya Dunia na shirika la fedha duniani IMF na kuwezesha baadhi ya madeni ya nje ya Tanzania kufutwa. Aidha Mhe. Mkapa alifanya juhudi za kupambana na ufisadi zilizopelekea kuundwa kwa jukwaa la wazi lililoitwa Tume ya Rais juu ya ufisadi iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Sinde Warioba na kuongeza msaada katika mapambano hayo.

Awamu ya nne ya Dkt Jakaya Mrisho Kikwete ilikuja na dira ya maisha bora kwa kila mtanzania kwa kuzingatia anapitia na kuboresha kila sekta ili watanzania wote wanufaike na nchi yao kwa kuwa na maisha bora kwanzia daraja la juu mpaka wananchi wa daraja la chini. Mipango hiyo ilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kwani watanzania wengi maisha yao yalibadilika na kuwa bora.  Maboresho yalifanyika kwenye sekta ya ulinzi na usalama, huduma za kijamii na sekta ya utalii  pamoja na uwekezaji sekta nyengine muhumu zenye kuleta maendeleo chachu kwa maisha bora ya watanzania.

 Rais wa awamu ya tano wa Jamuhuri ya Muungano wa tanzania Dkt John Pombe Magufuli kupitia sera ya HAPA KAZI TU ametekeleza dira alizoziweka tangu aanze kuhudumu katika kipindi chake na kuhakikisha dira zilizowekwa na Maraisi wa awamu zilizopita zinafikiwa kikamilifu.

Katika kukamilisha sera na dira yake Rais Magufuli anaamini kwamba viwanda vitakua nguzo katika taifa ili kuleta uchumi ulio bora huku ukitengeneza ajira kwa Watanzania wengi. Rais Magufuli amezidi kujikita katika misingi ya baba wa Taifa katika kujenga vituo vingi vya afya ili kutokomeza adui ambae ni maradhi, kaboresha shule nyingi na kujenga na ameweza kutekeleza sera ya Elimu Bure ili kila mtoto wa kitanzania aweze kusoma.

Sambamba na hayo Shauri aliongelea Viongozi wakubwa Duniani ambao walikua na dira katika uongozi wao zilizosababisha kufikia mafanikio viongozi hao ni pamoja na  Mao Zedong wa China, Mahatma Gandhi wa India  na Martin Luther King wa Marekani.

Mahatma Gandhi alikuwa mwanasheria, mwanafalsafa na mtetezi wa haki za binadamu na kiongozi wa juu wa siasa nchini India.Ghandi alifanya kazi kwenye shamba la miwa nchini Afrika Kusini  lakini aliweka dira kwamba akirudi nchini kwake atahakikisha India inapata uhuru. Aidha aliporejea India aliweka mipango ya kimkakati kwa kutumia mbinu ya uasi wa kiraia usio wa vurugu ulioisaidia india kupata uhuru na kuhamasisha mavuguvugu kadhaa ya haki za kiraia na uhuru Duniani.

Naye Mao Zedong alikua ni kiongozi wa Jamhuri ya watu wa China  kuanzia mwaka 1949 na kiongozi wa chama cha kikomunisti cha China tangu 1935 hadi kifo chake 1976. Katika hatua za mwanzo siasa yake ya kiuchumi ilisababisha njaa na vifo vingi wakati wa utekelezaji lakini maono na ndoto za Mao zilikua ni kuipeleka China katika uchumi ambao sasa tunauona. China imekua nchi ambayo ina uchumi wa juu kutokana na sera iliyowekwa na Mao.

Martin  Luther King alikua na dira na ndoto kuwa ipo siku moja Marekani itaongozwa na mtu mweusi na ndoto hiyo ilitimia kwani mnamo mwaka 2009 hadi mwaka 2017 Nchi ya marekeni iliongozwa na mmarekani mweusi Barack Hussein Obama akiwa kama raisi wa awamu ya 44 kupitia chama cha Democratic.

HITIMISHO

Katika kuhitimisha sehemu hii ya kwanza ya makala Mkurugenzi Jumanne Shauri ametolea  mfano jinsi kiongozi wa Taifa letu Dkt. John Pombe Magufuli ametekeleza Dira kwa vitendo baada ya kuahidi kufika kwenye uchumi wa kati  kabla ya mwaka 2025 na hatimaye kufikia malengo hayo ndani ya mwaka 2020, na kusema kuwa hayo yote yamewezakana ndani ya muda mfupi kutokana na ukweli kuwa kiongozi wetu wa Nchi  alipoingia tu madarkani aliingia na sera yake ya HAPA KAZI tu na kuja na mipango ya kimkakati ya kutimiza sera hiyo kwa kuanzisha na kufufua viwanda ili kutoa fursa ya ajira kwa kila mtanzania.

 

Aidha Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Jumanne  Shauri amezishauri Manispaa kuwa zinaweza kuweka dira ya kujitegemea na kujiendesha kwa mapato binafsi kwani mpaka sasa kuna baadhi ya Manispaa zinajiendesha zenyewe kwa zaidi ya asilimia ishirini (20%)  hivyo wanaweza kuweka dira ya kujitegemea kwa zaidi ya hapo.

10 Desemba 2020

Madiwani wa Ilala Waapishwa katika ukumbi wa Anatoglou

 Na Mariam Hassan

Katika ukumbi wa Anatoglou wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala leo mapema asubuhi kumefanyika  Uzinduzi wa baraza la Madiwani pamoja na uapishwaji wa Madiwani.Baraza hilo liliongozwa na Mwenyekiti Katibu Tawala Wilaya ya Ilala Bi.Charangwa Selemani aliwapongeza madiwani kwa kuchaguliwa tena na kuwasisitiza kutimiza ahadi zao walizowaahidi wananchi.

Hakimu Mkazi Mahakama Kuu  ya Sokoine Drive Mh. Aziza Kalli aliongoza zoezi la uapishaji madiwani wote, na pia madiwani walifanya uchaguzi wa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala ambaye aliyechaguliwa ni Mh. Omary Kumbilamoto diwani wa Kata ya Vingunguti aliyepita kwa kura zote asilimia 100%, pia walifanya uchaguzi wa Naibu Meya ambaye aliyechaguliwa ni Mh. Saady Khimji diwani wa Kata ya Ilala naye alipita kwa kura zote asilimia 100%.


                                                                            Baadhi ya Madiwani wakila kiapo                           Mbunge wa Ukonga Mh. Jerry Silaa akisikiliza kwa makini


Aidha, Mstahiki Meya Mh. Omary Kumbilamoto alitoa shukurani zake kwa madiwani wenzake kwa kumchagua kushika nafasi hiyo na kuwaahidi kuwa atashirikiana nao kwa kila shughuli ili kuleta maendeleo katika Manispaa ya Ilala, naye Naibu Meya Mh. Khimji alitoa shukurani zake kwa madiwani na kuahidi kushirikiana nao pamoja na Mstahiki Meya na Mkurugenzi ili kuleta maendeleo katika Manispaa.           Mh. Omari Kumbilamoto ambae alichaguliwa kuwa Meya akitoa neno la shukraniPamoja na hayo madiwani waliunda Kamati za kudumu na kuchagua wenyeviti na wajumbe wa kamati hizo.

Katika kikao hicho cha Baraza la madiwani wananchi kutoka sehemu mbali mbali pamoja na Mashirika Binafsi walihudhuria.                          Baadhi ya Wananchi waliofika katika ukumbi wa Anatoglou