27 Novemba 2020

Halmashauri ya Manispaa ya Ilala yaadhimisha siku ya Mlipa Kodi

 Na,Rosetha Gange 

Halmashauri ya Manispaa ya Ilala  imeadhimisha siku ya mlipa kodi ikiambatana na utoaji wa elimu kwa mlipa kodi na ugawaji wa tuzo kwa wafanyabiasha na taasisi mbalimbali ambazo ni vinara wa kulipa Kodi na kuchangia mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.

Akihutubia katika hafla hiyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala Ndg. Jumanne Shauri aliwapongeza na kuwashukuru wafanyabiasha wote kwa mchango wao mkubwa kwa Manispaa ya Ilala kwani kupitia Kodi wanazolipa,Serikali inaweza kutekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo mfano, ujenzi wa Barabara, zahanati na madarasa. Pia kupitia Kodi wanazotoa wafanyabiasharara wengine na wajasiriamali wadogo wanaweza kukopeshwa mitaji na kukuza biashara zao hivyo kuongeza mapato ya Halmashauri na kuleta maendeleo ya Taifa letu.

Akinukuu maneno ya Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh .Dr. John Pombe Magufuli kuhusu maendeleo ya nchi yetu alisema

 "Hakuna mtu atakayetusaidia maendeleo yetu Watanzania.Maendeleo yetu watanzania tutayajenga sisi wenyewe kwa kutumia Kodi zetu wenyewe."

Aidha, amewataka walipa kodi hao kuendelea kulipa Kodi kwani ni kitendo cha kizalendo na tuzo hizo walizopewa ziwe ni chachu ya kuendelea kuchangia mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala hivyo kuleta maendeleo katika taifa letu.

Akitoa salamu za Serikali mgeni Rasmi katika hafla hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mh.Ng'wilabuzu Ludigija alitoa pongezi kwa wafanyabiashara wote waliopata tuzo hizo na kuwaomba wakawe mabalozi kwa wafanyabiashara wengine.Vilevile amewaahidi ushirikiano pale watakapokuwa na matatizo yoyote ofisi yake itakuwa tayari kuwasikiliza na kushughulikia ipasavyo.

Aidha, ametoa rai kwa wafanyabiashara wote nchi nzima kufuata mifumo rasmi ya ukusanyaji kodi iliyowekwa na serikali na sio kutumia watu wengine wa katikati ambao wanaweza kutumia njia za udanganyifu na mwisho kujikuta wanaingia matatani.

Mapato ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala yameweza kuongezeka kwa 10% ndani ya kipindi Cha miaka mitatu kutoka Billioni 46 mwaka 2017/2018 mpaka Bilioni 57 mwaka 2019/2020 na matarajio ya mpaka kufikia mwaka 2025 ni kukusanya Bilioni 100.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni