24 Oktoba 2020

Mahafali ya 18 Shule ya Msingi Diamond yafana

 Na: Hashim Jumbe

Siku zimepita na miaka imekwenda, hatimaye ile siku iliyokuwa ikingojewa  kwa hamu ikawadia, ni siku itakayobaki kukumbukwa na wazazi, wanafunzi na walimu wa shule ya msingi Diamond, ni siku niifananishayo na ile iliyotajwa na Muandishi Ben R. Mtobwa kwenye Riwaya ya 'Zawadi ya Ushindi' siku ambayo muhusika Sikamona anarudi kutoka vitani na kukabidhiwa zawadi aliyoahidiwa na mchumba wake Rusia, nayo ni zawadi ya ushindi.

Miaka Saba (7) ya elimu ya msingi imetamatika kwa vijana walioianza safari yao ya kielimu mwaka 2014, ambapo siku ya leo imekuwa ya furaha huku bashasha zikitawala kwenye nyuso zao wakati wa mahafali ya 18 ya kuwaaga yaliyofanyika leo katika shule ya msingi Diamond.

"haikuwa kazi rahisi kwa vijana hawa, nakumbuka mwaka 2013 wakati tunawafanyia usahili waweze kuingia darasa la kwanza, walikuwa wadogo mno, wengine mpaka walikuwa wanapotea madarasa ya kufanyia mtihani, nashukuru leo nimewaona wakiwa wakubwa na furaha yangu ni kwamba wameweza kutuletea heshima kwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao ya utimilifu, lakini naamini na mtihani wa Taifa watakuwa wamefanya vizuri pia" Bi. Elizabeth Thomas, Afisa Elimu Msingi Manispaa ya Ilala

Aidha, mahafadhi ya 18 yaliyofanyika kwenye viwanja vya shule hiyo ya Diamond, yalichagizwa na burudani kutoka kwa wanafunzi waliohitimu shuleni hapo na yakahitimishwa na utoaji zawadi mbalimbali kwa wanafunzi waliofanya vizuri kwenye taaluma, michezo, nidhamu na uongozi bora


Maoni 1 :

  1. Safi Sana mwalimu mkuu Bora kabisa kuwahikupita hapo diamond primary school,tunashukuru kwa watoto wetu kuwalea na kuwafanya kuwa Bora kwenye masomo

    JibuFuta