30 Septemba 2020

WALIMU ILALA WAKUTANA KIKAO KAZI

 


Na; Hucky Hamis na Shamimu Msuya

Halmashauri ya Manispaa ya Ilala imewakutanisha walimu wote wa shule za msingi katika Manispaa hiyo siku ya Jumanne 29. 09. 2020 kwenye Kikao Kazi cha awamu ya tatu kilichofanyika kwenye ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere, Posta jijini Dar es Salaam ili kujadili mafanikio na kutatua changamoto za walimu hao.
                                             Baadhi ya Walimu waliofika kwenye Kikao Kazi


Kadhalika, Afisa Elimu wa Manispaa ya Ilala Bi. Elizabeth Thomas ametanguliza shukrani na pongezi za dhati kwa walimu hao kwa majukumu wanayofanya katika kufundisha na kuhudumia wanafunzi wa aina zote jambo ambalo limeifanya Manispaa hiyo kuwa kwenye nafasi za juu kitaaluma na kueleza kuwa tangu mwaka 2015 kumekuwa na ongezeko kubwa la idadi ya uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza, kuimarika kwa miundombinu ya shule ikiwemo nyumba za walimu na upatikanaji wa maji na ongezeko la samani za shule ambazo zimetolewa na Benki ya CRDB ambao ni wadau wa elimu.

Aidha, Walimu walipewa nafasi ya kuuliza maswali na kutoa changamoto wanazopitia ambapo Mwalimu Henry alizungumza juu ya changamoto wanazopitia kwenye ulipwaji wa posho za likizo.

Akijibu changamoto hiyo, Afisa Utumishi wa Manispaa ya Ilala Bwana Said Ismail amesema  “Kwanza niwatoe wasiwasi walimu wangu kwasababu hiyo changamoto ipo kwenye hatua za ufumbuzi na linashughulikiwa na TAMISEMI kwa kuwa imekuwa ni changamoto kubwa na siyo changamoto yenu walimu pekee bali ni kwa watumishi wote, kwahiyo tuwe wavumilivu wakati jambo hili linashughulikiwa”

            Afisa Utumishi wa Manispaa ya Ilala Bw. Said Ismail akijibu changamoto za kiutumishi


Sambamba na hayo, suala la upashanaji habari kati ya wananchi na serikali halikuachwa nyuma ambapo Afisa Uhusiano wa Manispaa ya Ilala kutoka kitengo cha Habari, Uhusiano na Mawasiliano Bi Tabu Shaibu amesema “Napenda kuwakaribisha walimu wetu wa elimu msingi kufanya kazi na sisi kwani sisi ni daraja kati ya vyombo vya habari na wananchi, lakini idara ya Elimu Msingi inajitahidi  na kunifanya nionekane nafanya kazi sana” aliendelea kwa kuwakaribisha sana walimu kushirikiana na idara ya habari ya Manispaa katika kutatua changamoto za ndani badala ya kutumia vyombo vya nje ili kusaidia kupata ufumbuzi kwa haraka zaidi.

Pia, Afisa Elimu Msingi wa Manispaa Bi. Elizabeth Thomas alimalizia mjadala kwa kuwakumbusha walimu kujiandaa kustaafu ili kuepusha changamoto wanazokutana nazo baada ya kustaafu wakiwa hawajajiandaa ikiwemo kuandika miaka sahihi na kujipanga kimaisha na mwisho kumkaribisha Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Bwana Jumanne Shauri kufunga kikao hicho na alifunga kwa kuwatia moyo walimu kuwa wajivunie kuwa na taaluma hiyo kwani ni miongoni mwa taaluma ambazo hazina mwisho wa kufanya kazi.

Kikao kazi hicho cha Manispaa ya Ilala Idara ya Elimu Msingi hufanyika mara moja kila mwaka na mwaka huu 2020 kimefanyika tarehe 22, 28 na 29 Septemba kikihusisha jumla ya walimu 3,700 wa Manispaa ya Ilala na kufayika kwa awamu tatu.

 

 

 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni