8 Desemba 2017

MANISPAA YA ILALA YAWAAPISHA WENYEVITI NA WAJUMBE WA KAMATI ZA MITAA, MKURUGENZI AWAASA KUSIMAMIA HAKI

Na: Hashim Jumbe
Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, leo imewaapisha Viongozi wake wa Mitaa ambao ni Wanyeviti wapya 12 wa Kamati za Mitaa pamoja na Wajumbe 35 wa Kamati za Mitaa.Viongozi hao wapya wametokana na kuchaguliwa kwenye Uchaguzi mdogo uliofanyika tarehe 16 Novemba, 2017 ikiwa ni kuziba nafasi zilizoachwa wazi kwenye Mitaa hiyo 12 kutokana na sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufariki kwa Wenyeviti waliokuwepo awali na wengine walioondoka kwenye nafasi zao na kwenda kutumikia nafasi nyengine.

Kiapo hicho cha Utii na Uadilifu kwa Viongozi hao wa Mitaa, ni maelekezo ya Kanuni za Uchaguzi wa Mwenyekiti wa Mtaa na Wajumbe wa Kamati za Mtaa katika Mamlaka za Miji za mwaka 2014 Ibara ya 30, kifungu cha 2.

Aidha, ikumbukwe Mitaa iliyokuwa ikifanya Uchaguzi huo ni Mitaa 12 kutoka kwenye Kata 7 za Manispaa ya Ilala, na Mitaa hiyo ni;- Bonyokwa, Twiga, Relini, Kasulu, Mongolandege, Amani, Kitinye, Machimbo, Kipunguni B, Kivule, Kerezange na Bombambili.

Akiongea wakati wa zoezi hilo la kula kiapo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Ndugu Msongela Palela aliwaasa Viongozi hao wa Mitaa kwenda kutenda haki kwa Wananchi waliowachagua "nyinyi ni Viongozi wa kuchaguliwa  na Wananchi, wamewachagua nyinyi kwa kuwa wana imani kubwa kwenu. Wanaamini kuwa mtakuwa Viongozi katika kutatua changamoto zinazowakabili, lakini pia mtakuwa Viongozi katika kutoa na kuibua Mipango ya Maendeleo katika maeneo yenu ya Utawala"

Mwisho, Mkurugenzi Palela alitoa rai kwa Viongozi hao "natoa rai kwenu, kuwa mnapaswa kutekeleza wajibu na majukumu mliyokasimiwa na Wakazi katika Mitaa yenu kwa Utii na Uadilifu mkubwa"
Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala, Ndugu Msongela Palela akiongea na Wenyeviti pamoja na Wajumbe wa Kamati za Mitaa kabla ya kuanza zoezi la kuwaapisha
Mwanasheria Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Wakili Bonaventure Mwambaja akitoa muongozo wa kiapo cha Utii na Uadilifu namna kinavyokuwa na masharti yake
Mwanasheria Mkuu wa Manispaa ya Ilala, Wakili Mwambaja akiongoza Kiapo cha Utii na Uadilifu kwa Wenyeviti wapya wa Kamati za MitaaKatibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Ndugu Edward Mpogolo akitoa nasaha zake kwa Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati za Mitaa mara baada ya kula kiapo

7 Desemba 2017

DC-MJEMA AKABIDHI GARI YA KUBEBEA WAGONJWA HOSPITALI YA CHANIKA NA KISHA AWAJULIA HALI WAMAMA WALIOJIFUNGUA

Na: Hashim Jumbe
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Sophia Mjema amekabidhi gari ya kubebea Wagonjwa kwenye Hospitali ya Mama na Mtoto Chanika (Korea-Tanzania Friendship Maternity Hospital). Gari hiyo yenye thamani ya Shilingi Milioni 140 limenunuliwa kutoka kwenye Mapato ya ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala.

Makabidhiano ya gari hilo la Wagonjwa yanakamilisha mahitaji yote muhimu katika Hospitali hiyo ya Mama na Mtoto baada ya uwepo wa vifaa tiba, nyumba ya Watumishi pamoja na uwepo wa Watumishi wenyewe.

Wakati wa kukabidhi gari hiyo, Mhe. Sophia Mjema alipata pia fursa ya kukagua shughuli zinavyoendelea hospitalini hapo na kisha kusalimiana na Wamama waliojifungua.
DC-MJEMA AZINDUA JENGO LA WAZAZI ZAHANATI YA MVUTI BAADA YA KUFANYIWA MAREKEBISHO

Na: Hashim Jumbe
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Sophia Mjema amefanya uzinduzi wa jengo la Wazazi katika Zahanati ya Mvuti baada ya kufanyiwa marekebisho yaliyogharimu jumla ya Shilingi Milioni 69.5 ambapo Wananchi wa Mtaa wa Mvuti walichangia Shilingi Milioni 20.1 na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala ilichangia Shilingi Milioni 49.5.

Aidha, Zahanati ya Mvuti iliyoanzishwa mwaka 1976 inahudumu jumla ya Wakazi wapatao 24,461 huku jengo hilo la wodi ya Wazazi lililoanzishwa mwaka 2013 kwa jitihada za Wananchi pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Ilala limeweza kupunguza msongamato na kufanya upatikanaji wa huduma kwa Mama kuwa katika mazingira mazuri
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Sophia Mjema akiongoza kwenye ukataji utepe ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa jengo la Wazazi kwenye Zahanati ya Mvuti baada ya kufanyiwa marekebisho
Jengo la akina Mama lililofanyiwa ukarabati kwenye Zahanati ya Mvuti linavyoonekana baada ya ukarabatiMkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Sophia Mjema akikagua wodi ya Wazazi baada ya kufanyiwa ukarabati

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Sophia Mjema akiwa na mmoja ya Watoto waliowahi kuzaliwa kwenye Zahanati ya Mvuti 

6 Desemba 2017

MKUU WA WILAYA YA ILALA AZINDUA JENGO LA MAMA NA MTOTO ZAHANATI YA MSONGOLA, APOKEA NA VIFAA TIBA TOKA BENKI YA TIB

Na: Hashim Jumbe
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mhe. Sophia Mjema amezindua jengo la kutolea huduma ya Mama na Mtoto kwenye Zahanati ya Msongola, iliyopo Mtaa wa Yengayange pembezoni mwa Manispaa ya Ilala, huku ujenzi wa jengo hilo ukigharimu Jumla ya Shilingi Milioni 106.5 ambapo Shilingi Milioni 91.5 ni ufadhili kutoka Shirika la Kimataifa la Pathfinder na Shilingi Milioni 15 ni mchango wa Wananchi wa Kata ya Msongola.

Sanjari na uzinduzi wa Jengo hilo, lakini pia Mkuu huyo wa Wilaya ya Ilala alipokea na vifaa tiba vyenye thamani ya Shilingi Milioni 7 kutoka Benki ya TIB ili kuhakikisha huduma zinazotolewa kwenye Zahanati hiyo zina ubora unaostahili ikiwa ni pamoja uzazi bora na salama.

Vifaa tiba vilivyotolewa na Benki ya TIB ni pamoja na; Delivery beds-3 section with mattresses-2pcs, Delivery kit-superior quality 1 pc, Suction pump foot/hand operated 600 ml (twin) 1 pc, Blood pressure machine-Mobile Aneroid 1 pc, Blood pressure Machine-Digital 1 pc, Blood pressure machine-Aneroid 1 pc.

Zahanati hiyo ya Msongola iliyoanzishwa mwaka 1975 inahudumia Wakazi wapatao 24,461 kutoka maeneo yote ya Mtaa wa Yangeyange na Mitaa ya jirani kama vile Mbondole, Kitonga, Mvuleni na Mitaa ya Kisewe na Mbande iliyopo upande wa Manispaa ya Temeke, hivyo upatikanaji wa Jengo hilo pamoja na vifaa tiba utawarahisishia Wakazi wa maeneo hayo kupata huduma ya haraka
Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Sophia Mjema sambamba na Mbunge wa Jimbo la Ukonga Mhe. Mwita Waitara wakipokea vifaa tiba kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya TIB Bw. Edward Lyimo wa kwanza kulia. Vifaa hivyo ni msaada kwaajili ya huduma za Mama na Mtoto
Wodi ya Mama na Mtoto kwenye Zahanati ya MsongolaMkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Sophia Mjema akizindua rasmi jengo la Wazazi kwenye Zahanati ya Msongola


Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mhe. Sophia Mjema akishikana mkono na Mbunge wa Jimbo la Ukonga Mhe. Mwita Waita ikiwa ni ishara ya kuunga mkono kwa pamoja juhudi za kuleta maendeleo kwa Wananchi wa Manispaa ya Ilala bila itikadi ya aina yoyote
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Kimataifa Pathfinder-Tz, Dkt. Joseph Komwihangiro akizungumza mbele ya Mgeni rasmi ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Ilala wakati wa uzinduzi wa jengo la kutolea huduma ya Mama na Mtoto kwenye Zahanati ya Msongola. Pathfinder walichangia Shilingi Milioni 91.5 kwenye ujenzi huo


15 Novemba 2017

KAMATI YA FEDHA NA UTAWALA MANISPAA YA ILALA YATEMBELEA MIRADI YA MAENDELEO ILIYOTEKELEZWA KWA KIPINDI CHA JULAI-SEPTEMBA,2017

Na:Hashim Jumbe
Kamati ya Fedha na Utawala ya Manispaa ya Ilala, imefanya ziara ya ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo iliyotekelezwa kwa kipindi cha robo ya kwanza ya kuanzia Julai hadi Septemba, 2017. Kamati hiyo iliyo na jukumu la kuhakikisha Miradi yote ya Maendeleo inayotekelezwa kwenye Halmashauri inapata usimamizi wa kutosha ikiwa pamoja na kupima thamani halisi ya fedha zinazotumika kwenye Miradi hiyo.

Wakati wa ziara hiyo, Kamati ya Fedha na Utawala ilipata nafasi ya kukagua Miradi mbalimbali ikiwemo ya Maji na Barabara. Miradi yote iliyotembelewa ni kama ifuatayo;
  1. Ujenzi wa Ofisi ya Serikali ya Mtaa Mvuleni iliyopo Kata ya Msongola; Ujenzi wa Ofisi hii utanufaisha Wananchi wapatao 2,141 ambao watapata huduma katika Ofisi hii, gharama za Mradi ni Shilingi Milioni 45.
  2. Ujenzi wa barabara ya Segerea-Bonyokwa iliyopo Kata ya Bonyokwa:  Kukamilika kwa ujenzi wa barabara hii utawarahisishia usafiri Wananchi waendao Bonyokwa, Segerea, Kinyerezi na Kimara. Gharama za Mradi ni Shilingi Bilioni 1.9
  3. Ujenzi wa Kisima na Miundombinu ya Maji; Ujenzi wa Mradi huu unatarajiwa kuwahudumia Wananchi wapatao 1,500 kutoka Kata ya Segerea. Gharama za Mradi ni Shilingi Milioni 53.5
  4. Ujenzi wa Jengo la Ofisi ya DMDP; Ujenzi huu wa jengo la ghorofa 3 kwa ajili ya Ofisi za DMDP. Gharama za Mradi ni Shilingi Bilioni 1.1 na Mradi huu utawanufaisha Watumishi kuwa na Ofisi nadhifu na mazingira yaliyoboreshwa kwenye kufanyia kazi.